Friday, July 17, 2015


Majeruhi wanane urais CCM       



                                    


Kwa ufupi
  • Sasa hawataweza kusubiri miaka kumi mingine kuwania tena kuingia Ikulu
  • Wasomi  wachambua hatima yao kisiasa baada ya wengi wao kuaga majimbo


Lowassa

Mchakato huo wa urais wa CCM ulitawaliwa na jina la Lowassa, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa baada ya harakati zake za kusaka wadhamini kuhudhuriwa na maelfu ya watu kuthibitisha kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa chama hicho kingechagua mtu anayekubalika ndani na nje ya CCM.

Lakini hakumudu kuingia tano bora na hivyo kuacha mgogoro mkubwa uliosababisha wajumbe wa Halmashauri Kuu kumuimbia Kikwete wimbo ulioonyesha kuwa wana imani na mbunge huyo wa Monduli.

Majeraha kwa waziri huyo mkuu wa zamani, pia yanaonekana kwenye kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alikuwa mstari wa mbele kumnadi na ambaye ameeleza wazi kuwa viongozi wa CCM walikula njama kumuengua.

Lowassa (62) pia alijitosa kwenye mchakato huo mwaka 1995 alipokwenda kuchukua fomu pamoja na Kikwete, lakini jina lake likaenguliwa.

Dk Bilal

Kada mwingine anayeonekana kuachwa akiwa na majeraha makubwa ni Dk Bilal, ambaye ni Makamu wa Rais. Bilal amepoteza nafasi ya kuendelea kushika nafasi hiyo baada ya mteule wa CCM, Dk John Magufuli kumpendekeza Samia Salim Suluhu kuwa mgombea mwenza. Kwa makamu wa Rais kutoingia tano Bora ni pigo kubwa.

Dk Gharib (70) aligombea urais wa Zanzibar mwaka mwaka 2010 na kushindwa, lakini CCM ikamteua kuwa mgombea mwenza wa Kikwete baada ya Dk Mohamed Shein kuteuliwa kugombea urais wa Zanzibar. Atakuwa akiuguza majeraha kwa kuwa mtu wa kwanza kushikilia nafasi hiyo kwa kipindi kimoja tangu siasa za ushindani zirejeshwe nchini.

Membe

Kundi lililoachwa na majeraha pia linamjumuisha Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye ameaga sehemu mbalimbali alizokuwa zikimhusu kutokana na kazi yake ya kisiasa na hasa jimboni kwake ambako tayari Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye ameshachukua fomu.

Membe (62) amefanya wizara hiyo kwa takriban miaka minane na alikuwa mmoja wa makada waliokuwa wanapewa nafasi kubwa. Alipenya kwenye tano bora, lakini akashindwa vibaya kwenye kura za wajumbe wa Halmashauri Kuu na sasa atakuwa akitafakari upya hatma yake kisiasa.


Pinda
Waziri Mkuu, Pinda naye ameachwa na majeraha. Ameingia kwenye orodha ya watu walioshika cheo hicho na ambao wamejaribu kuwania urais na kuenguliwa mapema.

Machungu ya kuenguliwa Pinda (67) pia yanatokana na ukweli kuwa alikuwa mtendaji mkuu wa Serikali na hivyo ilikuwa rahisi kushauriwa kutojiingiza kwenye mchakato kama hakuwa na nafasi hata ya kuingia tano bora.

Mbunge huyo wa Katavi ameshatangaza kuachia jimbo hilo na baada ya matokeo hayo, mustakabali wake utategemea busara ya viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Profesa Mwandosya

Mchakato huo pia umeacha jeraha katika jaribio la pili la Profesa Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), la kuwania urais baada ya mwaka 2005 kushika nafasi ya pili nyuma ya Kikwete aliyeongoza na Dk Salim Ahmed Salim.

Profesa Mwandosya, kama baadhi ya makada walioenguliwa, ameshatangaza kutogombea ubunge Jimbo la Rungwe Mashariki, hali ambayo imesafisha njia ya kuelekea kustaafu siasa baada ya kushindwa kwenye mbio za urais.

Sitta

Spika huyo wa Bunge la Tisa na pia Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, anaingia kwenye orodha ya majeruhi wa mchakato wa urais wa CCM baada ya kujiandaa kwa muda mrefu kuwania nafasi hiyo.

Sitta alisema bayana wakati alipochaguliwa kuongoza chombo hicho cha kihistoria cha kuandika Katiba kuwa atatumia uspika wake kutengeneza mazingira ya kuteuliwa na CCM kugombea urais.

Lakini naye hakupenya hata kwenye tano bora na inaelekea hatua inayofuata ni kwenda Tabora kutetea jimbo lake.

Akiwa na umri wa miaka 73, mwanasiasa huyo mkongwe sasa hana nafasi ya kugombea tena urais baada ya miaka 10 atakapokuwa na umri wa zaidi ya miaka 80.





Sumaye

Waziri Mkuu huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu, atakuwa akiuguza majeraha ya kupoteza nafasi ya kuteuliwa kwa mara ya pili baada ya jaribio lake la kwanza mwaka 2005 kugonga mwamba.

Alishaachana na siasa za majimbo tangu mwaka 2005 baada ya kukosa urais na akiwa na umri wa miaka 65, haiyumkini kuingia tena kwenye mbio za urais mwaka 2025.

Wasira

Waziri huyo wa Kilimo, Chakula na Ushirika, alitangaza awali kuwa asingegombea ubunge wa Bunda, lakini akabadilisha uamuzi huo licha ya kuingia kwenye mbio za urais. Wasira, ambaye mwaka huu ametimiza miaka 70, atakuwa akiwania kurejea bungeni akipambana na mwanasiasa kijana ndani ya CCM, Esther Bulaya.

 “Ni wazi kwa waliokuwa na matumaini makubwa ya kushinda ni pigo sana kuangushwa. Hata matamshi yao yalikuwa wazi kuwa walikuwa na uhakika hata walidiriki kusema ‘jina langu halitakatwa’ na mbio zao za kutafuta wadhamini zilikuwa ni za kishindo,” alisema Profesa Gaudence Mpangala, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco).

Profesa huyo wa masuala ya siasa na utawala, alisema kwa hali ya kawaida wagombea hao wameathirika kisaikolojia, hivyo hata wale waliokuwa wametangaza kutogombea wanaweza kubadili msimamo na kurudi kutetea majimbo yao.

“Magufuli akipata urais anaweza kuwafikiria hata uwaziri na iwapo upinzani watashinda, hali yao kisiasa ndiyo basi tena. Siasa siyo kazi ya kudumu, bali ni ya muda tu wa kuwatumikia wananchi ukimalizika, unastaafu.”


















No comments:

Post a Comment